“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu,
Oktoba 7, 2024
Juma la
27 la Mwaka wa Kanisa
Kumbukumbu
ya Bikira Maria wa Rozari
Gal 1: 6-12
Zab 111: 1-2, 7-10
Lk 10: 27-37
ROZARI:
TAFAKARI NA SALA ILIOJIKITA KATIKA KRISTO !
Wengi
wetu tunasali rozari wenyewe, katika jumuiya au katika familia lakini huenda
mara nyingi hatujui maana yake na umuhimu wake. Mt. Papa Yohane Paulo wa pili
katika barua yake ya Kitume “Rozari ya Bikira Maria” anasema “Rozari, ingawaje
ina tabia ya Maria, katika moyo wake ni sala iliojikita katika Kristo. Ina kina
cha ujumbe wa Injili katika hali yake yote. Ina sauti ya Maria, wimbo wake wa
daima kwa kazi ya ukombozi-umwilisho ilioanza ndani ya tumbo lake…..”.
Kielelezo cha Rosari ni juu ya Yesu-kuzaliwa kwake, maisha yake, kifo na
ufufuko. Sala ya ‘Baba Yetu’ inatukumbusha kwamba Baba yake Yesu ndiye chanzo
cha Ukombozi. ‘Salamu Maria’ inatusaidia kuungana na Maria kutafakari mafumbo
hayo. Inatusaidia kutambua pia Maria alikuwepo na ameunganika na Mwanae katika
mafumbo yote duniani na uwepo wake Mbinguni. ‘Atukuzwe Baba’ inatukumbusha kwamba umuhimu wa maisha yote
ni kwa ajili ya utukufu wa Utatu Mtakatifu. Hivyo, Rozari inatusaidia
kutafakari juu ya umuhimu wa mafumbo ya wokovu wetu.
Rosari
inapaswa ituguse sisi. Ni rahisi. Kurudia kwa maneno kila mara inatusaidia
kujenga hali ambayo tutatafakari mafumbo ya Mungu. Tutambue kuwa, Yesu na Maria
wapo nasi katika furaha na uchungu katika maisha yetu. Tumuombe Bikira Maria
atuombee tuweze kujenga tabia ya ndani ya kusali rosari kila siku. Hii ni
nyenzo ya sala zetu zote: tufikie mahali ambapo “tutasali bila kuchoka” kama
Mtakatifu Paulo alivyosema.
Leo katika Injili mwalimu wa sheria anamuuliza Yesu swali ambalo, sisi tungeweza kujiuliza katika maisha yetu ya kila siku. “Bwana, nifanye nini niurithi Ufalme wa milele?” (Lk 10: 25). Yesu, lakini, tena katika hekima anajibu kwa yale yalioandikwa katika Maandiko: ‘kumpenda Bwana Mungu wako na jirani yako kama nafsi yako’ (rej. Lk 10: 27). Kupenda maana yake ni kujitoa kwa wengine kwa yote tulio nayo na yote jinsi tulivyo.
Kujitoa kusikiliza wengine kujitoa kuelewa wengine na kuwa na subira kwa ajili ya wengine. Huo ndio upendo. Upendo huu unakuwa na asili ya Kimungu tunapo ueneza zaidi kwa wale walio tuumiza katika maisha au kwa wengine tusio waona hata macho kwa macho. Upendo unakuwa na Mguso wa Kimungu tunapo toka njee kwenda kuwasaidia hata watu tusio wafahamu. ‘Kama mtu mmoja anateseka, watu wote wanateseka naye, kama mmoja anaheshimiwa, watu wote wanashiriki katika furaha yake’ (1 Kor 12: 26). Hii ndio fadhila ya Msamaria Mwema.
Sala:
Ee Bikira Maria, niombee ili kusali rozari kila siku iwe tabia yangu, katika
harakati ya shughuli zangu mbali mbali, muunganiko wa umoja katika matendo
yangu, tabia ya muunganiko mtakatifu, kiburudisho kamili, hali ya kutia moyo
ili kutembea kwa furaha katika njia ya majukumu yangu. Amina
Copyright
©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment