Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUBADILI MAVAZI!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi, Oktoba 12, 2024
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa

Gal 3: 22-29;
Zab 104: 2-7;
Lk 11: 27-28


KUBADILI MAVAZI!


Somo la kwanza linatukumbusha sisi, Wakristo wabatizwa, kwamba katika ubatizo tulivalishwa vazi ambalo ni Kristo. Imani katika Kristo ilitubatiza ‘ndani ya Kristo’. Ubatizo huu wa Roho unamtambulisha mwamini na Kristo na unamfanya awe sehemu ya mwili wa Kristo. Ubatizo kwa njia ya maji ni ishara ya njee ya hii kazi ya ndani ya Roho Mtakatifu. Mwamini anapaswa atupilie mbali mavazi ya dhambi na kwa Imani, apokee mshipi na mavazi mapya ya haki yakumfunga ndani Kristo. Injili ya leo inauhusiano na Lk 8: 19-21, ambapo inaongelea kuhusu Mama na ndugu wa Yesu walitaka kumuona, inatoa somo lilelile kwamba mahusiano ya njee si zaidi ya kusikia neno la Mungu na kulitii. 

Kwa Injili ya Luka, Maria amebarikiwa kuliko wanawake wote. Lakini pia amebarikiwa kuliko wanawake wote si kwasababu ya kumzaa Mwana wa Mungu tu bali ni kwasababu aliliamini neno la Mungu na kulishika. Kwahiyo Yesu alivyosema wana heri zaidi wanao lishika neno la Mungu na kulitenda, Maria ni wakwanza kabisa tena kwa uaminifu mkubwa kulishika Neno la Mungu na kulitenda, hivyo Yesu haku maanisha kumtenga au kumkataa Mama yake. Wale wote wanaolisikia Neno la Mungu na kulitenda wanabarikiwa. Bikira Maria alivaa vazi la Imani isio yumba yumba na alijikabidhi kwa Mungu.

Kama isivyowezekana kulitenga Kanisa na Kristo, ndivyo isivyowezekana kumtenga Maria na Yesu. Yeye ni mfano unaongara katika kulishika Neno la Mungu. Maria anatufundisha jinsi ya kukubali na kulishika Neno la Mungu, jinsi ya kuliweka katika ubinadamu wetu, kuliishi, kuliweka ndani, nakulifanya lizae matunda mema. Kulifanya likue, na kuchukua sura mpya ndani mwetu, hata wakati tusipo lielewa au wakati linatufanya tuteseke. Wana heri wanaosikia Neno la Mungu na kulishika.

Sala: Bwana, tusaidie tuweze kuvaa vazi jipya la Upendo, huruma, haki na usawa. Amina


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment