Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

YESU NDIYE THAMANI YA KWELI!


“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Septemba 18, 2022 
Dominika ya 25 ya Mwaka


Amo 8:4-7
Zab 113: 1-2, 4-8
1Tim 2:1-8
Lk 16: 1-13


YESU NDIYE THAMANI YA KWELI!

“Kupenda pesa ni chanzo cha aina zote za uovu”(1Tim 6:10). Fedha zinaleta nguvu, kufurahia maisha na usalama lakini sanjari na hilo huweza kuwa chanzo cha tamaa mbaya, ubinafsi, wivu mbaya na aina mbali mbali za uovu katika maisha. Mara nyingi tumesikia vilio vingi kuhusu ubatilifu wa fedha, ufisadi, mauaji, wizi, na udanganyifu wa aina nyingi nk., mengi ya haya ikiwa ni katika harakati za kutaka kufanya maisha marahisi kwa njia za mkato. 

Katika Injili ya leo, tunakutana na mtu tajiri, aliyekabidhi biashara yake na vitu vyake kwa wakili wake. Lakini wakili huyu alitumia mali hizi ili kujitengenezea faida yake binafsi. Mkuu wake anafanya uamuzi wa kumwachisha kazi huyu wakili batili. Huyu wakili akiogopa usalama wake na maisha yake ya baadae, anafanya mpango na wadeni wa Bwana wake ili kupunguza katika akiba ili kujihakikishia usalama wa baadae. Hapa tunaona mtumwa anayeshindwa kumtumikia Bwana wake kwasababu alishakuwa mtumwa wa pesa, mali. 

Kila mtu anataka kuwa tajiri, kitu ambacho sio jambo baya. Utajiri wenyewe sio uovu, bali kupenda mno utajiri ni mbaya. Mtu anaweza kuwa mtumwa wa utajiri/mali kwa kuupenda mno. Kwahiyo, Yesu mwishoni mwa mfano huu anahitimisha mfano mzima kwa kusema “Hamwezi kutumtumikia Mungu na Mali” 

“Mafarisayo waliokuwa wapenda fedha, walisikia haya, wakamdhihaki”. Ilikuwa ni kwakipindi kufupi tuu kabla ya Yesu, wakati Herode mkuu alivyo likarabati na kuliongeza Hekalu la Yerusalemu, kwahiyo hali ya hekalu ilikuwa katika hali ya juu. Mafarisayo walitekwa na matajiri maarufu walioweza kutoa kiasi kikubwa cha fedha hekaluni. Tamaa ya mali iliwafanya watengeneze urafiki wa hali ya juu na matajiri tu na watu maarufu na kuwasahau maskini, wanyonge, wajane na yatima. Badala ya Mungu waka anza kutumikia mali (watu matajiri). Kwahiyo, kwa mfano huu Yesu aliwagusa moja kwa moja tena kwa uchungu na kwa njia hiyo wakamdhihaki. Pengine kwa wakati wetu linaweza kuwepo kati yetu, na ndio maana Papa Mtakatifu Fransisko anawakumbusha makuhani kila wakati wawe karibu na wanyonge katika jamii zetu, wasije wakanaswa na mtego huu wakuwapenda matajiri tuu na kuwasahau wanyonge.

Katika hali ile ile, katika somo la kwanza nabii Amosi anatuelezea athari za kuwa mtumwa wa fedha au mali. Amosi, nabii wa haki anatuonesha jamii iliyo jaa udanganyifu, ubatilifu na ufisadi uliyo kithiri. Mizani zili setiwa kwa udanganyifu, mshahara wa haki na wa wakati haukutolewa kwa maskini, matajiri wali wanyonya wanyonge na kutumia mali zao kwa ubinafsi wao. Ni zaidi ya miaka 2600 iliyopita, mwanadamu amestaraabika lakini baada ya miaka yote hii imekuwa vigumu kubadili haya. Wanyonge na wahitaji wame endelea kunyanyaswa na kudhulumiwa na kuonewa kwasababu tu ya ubinafsi na umimi wa wachache. Hawa wachache wamekuwa watumwa wa hela na mali, na kwa njia hii wanashindwa kutembea katika njia ya haki inayo oneshwa na Mungu. Sio waaminifu mbele za Mungu na sio waaminifu mbele ya jukumu lao kati ya wanadamu wenzao. 

Ndugu zangu, sisi nasi tunajikuta mara nyingi kama hawa, karani mjanja, mafarisayo na watu wakipindi cha nabii Amosi. Tumejaa uongo, tunadanganya, tuna batilisha mambo nk., ili kujijengea utajiri na usalama. Utajiri sio uovu lakini hatupaswa kujipatia utajiri kwa njia za uovu bali tupate utajiri kwa njia ya juhudi njema kwakufanya kazi na kwa haki. Pia tutambue hatuhitaji utajiri ili kujitegemeza bali kama Mt. Teresa wa Avila anavyosema “Mungu mwenyewe anatosha”. Tutakapo anza kuitumikia mali/fedha tunakuwa watumwa wasio na utashi mwema. Bali tutakapo anza kumtumikia Mungu, tunakuwa wakarimu na kuondokana na ubinafsi. Tujitahidi kutafuta Ufalme wa Mungu na kwa hakika kweli, mengine yote tutapewa kwa ziada.

Sala: Bwana, naomba uwe wewe tu thamani yangu na yote ninayo hitaji katika maisha yangu. Amina.


Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment