Jumanne, Septemba 13, 2022
Juma la 24 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mt. Yohane Chrisostom, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
1 Kor 12: 12-14, 27-31;
Zab 99: 2-5;
Lk 7: 11-17
TUTENDE KWA HURUMA!
Injili ya leo inatupa simulizi la kumfufua mtoto wa Mjane wa Naimu. Kwa maneno machache Luka anafanikiwa kutoa taswira nzuri ya jinsi pande zote mbili walivyokutana. Upande wa waliobeba mtoto aliyekufa (wafu) wa mjane wanaotoka njee ya mji kuelekea makaburini na upande wa Yesu (uzima) na umati unaomfuata wanaoingia mjini. Ni huruma iliomsukuma Yesu katika kusema na kutenda. Huruma hapa inaweza kutafsiriwa kama “kuteseka na” kujihisi au kufanya mateso ya mwenzako ni yako, kujitambua mwenyewe pamoja na mwenzako, kuhisi uchungu na mateso ya mwenzako. Ni huruma iliofanya nguvu ya Yesu iweze kutenda, nguvu ya uwezo wake juu ya kifo. Je, mateso, uchungu wa wengine unagusa roho yangu na kuwa na huruma? Je mimi nina saidia wengine waweze kuondokana na machungu yao na kujenga maisha mapya?
Leo tunamkumbuka Mt. Yohane Krisostom huyu anajulikana sana kwa kuinua maisha ya maadili ya mapadre na walei. Hakupendwa sana na wafalme wa enzi hizo na kwa njia hii alipelekwa uhamishoni mara mbili kwasababu ya uchovu na kukaukiwa alifariki. Mahubiri yake na maandishi yake yaliifafanua Imani na kuhimiza maisha ya Kikristo. Aliitwa Yohane Krisostom, maana yake ni Yohane mwenye mdomo wa dhahabu. Yeye ni mfano kwetu kwamba sisi nasi midomo yetu inapaswa kunena makuu ya Mungu sio kwa ajili ya kuwasema wengine na kuwaangamiza au kuwachafua. Bali midomo yetu iwe midomo ya dhahabu kama Mt. Yohane Krisostom ya kutangaza maneno ya Kristo kwakuonesha huruma na mapendo kwa watu wote kama Yesu alivyofanya kwenye Injili ya leo.
Sala: Bwana niinue tena, wakati nikiwa sina nguvu na nikiwa na mashaka. Amina
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment