Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA JUMAMOSI, SEPTEMBA 10, 2022


MASOMO YA MISA 
JUMAMOSI, SEPTEMBA 10, 2022
JUMA LA 23 LA MWAKA


KUMBUKUMBU YA JUMAMOSI YA BIKIRA MARIA

SOMO 1
1Kor. 10:14 – 22

Wapenzi wangu, ikimbeni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha Baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. Waangalieni hao waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?

Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilicholewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 116:12 – 13, 17 – 18 (K) 17

(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, Ee Bwana.

Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)

Nitalitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Katika nyua za nyumba ya Bwana,
Ndani yako, Ee Yerusalemu. (K)


SHANGILIO
Yn. 8:12

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, 
asema Bwana, yeye anifuataye 
hatakwenda gizani kamwe, 
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.


INJILI
Lk. 6:43 – 49

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.

Na kwa nini mnaniita, Bwana, walakini hamtendi nisemayo?

Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba yakawa makubwa.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment