Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA ALHAMISI, SEPTEMBA 15, 2022


MASOMO YA MISA 
ALHAMISI, SEPTEMBA 15, 2022
JUMA LA 24 LA MWAKA


KUMBUKUMBU YA BIKIRA MARIA MTAKATIFU WA MATESO


SOMO 1
Ebr. 5:7 – 9

Kristo, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa wa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mates ohayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 31:1 – 5, 14 – 15, 19 (K) 16

(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike mbele kwa haki yako uniponye.
Unitegee sikio lako, uniokoe hima. (K)

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kuniokoa,
Ndiwe genge langu na ngome yangu,
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. (K)

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu,
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu! (K)


SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Bikira Maria anafurahi yeye ameshinda na kupata nishani ya ushahidi pasipo kufa, alipokuwa chini ya msalaba wa Bwana.
Aleluya.


INJILI
Yn. 19:25 – 27

Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Au

INJILI
Lk. 2:33 – 35

Babaye na mamaye wa Yesu walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga ukaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment