Jumatatu, Septemba 23, 2024
Juma la 25 la Mwaka
Mit 3: 27-34
Zab 14: 2-5
Lk 8:16-18
JIPE MWANGA NA YESU
Wakati jua linapo zama na giza kuingia, mwanga unaleta tena maisha, na kunakuwa na mizunguko mingine na kazi huendelea. Yesu leo analiweka wazi, kumwamini yeye na kumfuata haipaswi kuwa na moyo nusu nusu na haipaswi kuwa kitu cha “siri” kwamba unakuwa unaona aibu kwasababu ya wengine. Kama wanafunzi wa Yesu hatupaswi kuwa na wasi wasi wowote au kuogopa wengine wanasema nini juu yetu. Hata hivyo, tunatafuta Amani, upendo, msamaha, haki na thamani ya Injili; tunapaswa kutembea tukiwa na ujasiri wote. Tujiringie kuwa wabebaji wa mwanga mkuu-YESU. Haijalishi tutapita katika giza lipi, ulimwengu wenye mashaka, sisi tunao mwanga wenye kuangaza njia zetu mpaka mwisho. Inaweza kuwa ngumu lakini tunapaswa kutembea katika mwanga huu tukifanya kazi na kusonga mbele. Mpaka pale tutakapo kuwa na mwanga huu milele, tusiogope na wala tusipoteze tumaini la mema tutakayo pata kwa hili.
Tukiwa na Mwanga huu, tutaenenda katika njia za hekima, kama somo la kwanza linavyo sema wazi wazi, kuenenda katika unyofu na kujitenga na choyo, kuwapa jirani zetu kile alichotupa Mungu. Ni wazi kwamba Mwanga na giza haviwezi kukaa pamoja kwa wakati mmoja, tujitahidi kubeba mwanga huu ili tuweze kujitenga na uovu na yote yasioendana na mwanga huu. Tuombe msaada wa Mungu ili tuweze kuuvaa mwanga huu ili tuweze kuwa kama mwanga wenyewe, kufanana na Kristo Yesu.
Sala: Bwana, tusaidie tuweze kuwasha mwanga wa mshumaa badala ya kulilaani giza. Amina
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment