Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

GHARAMA YA UFUASI!


“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Septemba 4, 2022 
Dominika ya Juma ya 23 ya Mwaka


Hek 9:13-16;
Zab 89:3-6, 12-14, 17;
Flm 1:9-10, 12-17;
Lk 14:25-33.


GHARAMA YA UFUASI!

“Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, mke wake, kaka na dada, naam hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” Lugha ya utangulizi ya Injili ya leo ni inaonekana kuwa ngumu sana. Ufuasi wa Mungu unamaana, kazi ya Mungu kwanza na mengine yote ya pili. Sio wote wanaweza kufurahia hili, hili linaelezea pia ni kwanini tuna wafuasi wachache wa Yesu. 

Kipindi cha Yesu kama kipindi chetu kuna watu waliotayari kila siku kufuata mambo mapya, mawazo mapya, aina za nguo mpya, fasheni hata katika dini. Kila mtu anaweza akasimama na kusema mimi ni mfuasi wa Yesu kwa madai amepata ufunuo wa maandiko. Ufalme wa Mungu lakini haujajengwa katika hisia bali katika kujikita katika uaminifu. Ufuasi una gharimu. Upo tayari kulipa gharama? 

Yesu anasema na anashauri kwamba, ufuasi wake sio ufuasi wakufuata kama kipofu. “kaa chini” alisema “Pima faida na hasara”. Usiseme ndio mpaka pale ninapofikiri nina hakika. Katika hali ya tofauti, dini nyingi, madhehebu na makundi ya Imani wanaamini kwamba dini ni kuhusu idadi ya watu. Yesu hataki wafuasi lelemama au wasioamua kutoka ndani. Yeye hatoi falsafa ya kucheza na maneno au ufalme wa kidunia, hapendi watu wafungwe katika kitu wasichoelewa. Yesu anahubiri uhuru. Wafuasi wake walitangaza uhuru. Hatuwezi kufanya hivyo kama sisi hatupo huru. 

Kama Yesu, tunapaswa kupanua mawazo yetu kuhusu familia na taifa. Neno familia linapaswa kubeba watu wote. Ujumbe wa Yesu ulikuwa ni kwa wote, hakuwa na watu maalumu kwaajili ya neno lake. Sisi mara nyingi tunajaribu kuweka yale mazurii kwaajili ya wale tunaowapenda na marafiki zetu. Wakati sisi kama wafuasi wa Kristo tunapaswa kutangaza injili kwa watu wote, kwasababu wote ni kaka na dada zake. 

Mfano wa kugusa kabisa katika hili unatoka katika barua kwa Filemoni. Paulo anaandika barua kwa niaba ya mtumwa aliyekimbia, Onesimo. Katika barua Paulo haandiki ili kuomba Onesimo arudi katika nyumba ile akaendelee na kazi yake kama mtumwa au ili asipewe adhabu bali Paulo anamuomba Filemoni ampokee Onesimo kama kaka yake. (Watalaamu wa Biblia wanasema kwamba huenda Onesimo alisoma barua kwa Wagalatia kwamba sisi sio watumwa tena tumekuwa huru katika Kristo, ndio maana alimtoroka Filemoni nakwenda Efeso ambako Paulo alifungwa Gerezani). Paulo anaandika akiwa na ujasiri juu ya ufuasi wa Filemoni kwamba anajua Filemoni atafanya makubwa zaidi hata ya yale aliomwomba. 

Mifano yote miwili katika Injili ya Luka leo, inaongelea kuhusu mambo yenye mantiki. Wa kwanza, ni kuhusu kuamua kujenga nyumba. Kuna kukaa chini, nakupanga, kuangalia uwezo wake wa kifedha na mambo mengine kabla hajaanza shuguli yake, kwani itakuwa ni ujinga kuanza msingi na baadae kuishiwa fedha. Mfano wa pili, unarudia ujumbe wa kwanza. Kama Nchi itaamua kwenda vitani, viongozi ni lazima wakae chini na kuangalia gharama. Au suluhisho sahihi ni kutuma ujumbe kuomba Amani. Ni katika hali hii hii Yesu anatutaka tukae chini, tuhesabu gharama za kuwa mfuasi wake, au sivyo tutaanza msingi wetu katika yeye na kama hatujui gharama yakumfuata tutaishia njiani. Ni lazima kutambua kumfuata yeye kuna majitoleo makubwa, kukataliwa hata na ndugu zako, au kuacha mambo ambayo dunia inadhani kila mwanadamu anapaswa kuwa nayo au kuyaishi. Kuacha baba, kaka na mengine kama Yesu alivyosema, alimanisha kwamba kitu chochote kisiwe kizuio cha kumfuata yeye, si mzazi wala ndugu yeyote wa karibu anaweza kukuzuia kumfuata Yesu. Yesu hakumanisha tusiwapende wazazi wetu bali alitaka tujue hata yale ambayo kwa akili zetu tunadhani ni ya kwanza, sio hivyo, bali katika kumfuata yeye lazima yeye awe wa kwanza na mengine yote yaje baadae. 

Wengi wanaanza kwa nguvu kabisa kumfuata Yesu, lakini Injili inavyozidi kuwapa changamoto, wanapotea na kuanza kutafuta Imani inayoweza kuwapa nafuu. Wanaanza kutembelea makanisa, vikundi vya sala, dhehebu moja baada ya jingine. Wanakuwa wakristo vuguvugu. Yesu anatuuliza leo kama tumeshaamua kwa ujasiri wote kumfuata. Anatualika tuwe na muda wakutafiti maisha yetu kila mara ili tuweze kuwa wafuasi wa kweli. 

Sala: Bwana Yesu, naomba unipe ujasiri wakuwa mfuasi wa kweli, anaye ishi injili na mwaminifu kwako katika nyakati zote. Amina


Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment