JUMAPILI, AGOSTI 24, 2025
DOMINIKA YA 21 YA MWAKA
SOMO 1
Isa 66: 18-21
Bwana asema hivi, Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi, na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa. Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, na katika magari, na katika machela, na juu ya nyumbu, na juu ya wanyama wepesi, mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu, asema Bwana; kama vile wana wa Israeli waletavyo sadaka yao nyumbani kwa Bwana katika chombo safi. Na baadhi ya hao nitawatwaa kuwa makuhani na Walawi, asema Bwana.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117 (K) Mk 16: 1512
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, Mkaihubiri Injili..
Aleluya.
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini. (K)
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SOMO 2
Ebr 12: 5-7, 11-13
Tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi. Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
SHANGILIO
Yn. 17: 17
Aleluya, aleluya,
Maneno yako ndiyo kweli, Ee Bwana,
Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya.
INJILI
Lk. 13: 22-30
Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment