Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, IJUMAA, AGOSTI 7, 2026




MASOMO YA MISA, IJUMAA, AGOSTI 7, 2026
JUMA LA 18 LA MWAKA

SOMO 1
Nah. 1:15; 2:2; 3:1-3, 6-7

Tazama juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye Amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali.

Kwa maana Bwana anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao.

Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang’anyi; mateka hayaondoki. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka; mpanda farasi akipanga, na upanga ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao. Nani nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dahrau. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji?

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


WIMBO WA KATIKATI
Kum. 32: 35 – 36, 39, 41 (K) 39

(K) Naua Mimi, nahuisha Mimi.

Maana siku ya msiba wao imekaribia,
Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.
Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake,
Atawahurumia watumwa wake. (K)

Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye.
Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi;
Naua Mimi, nahuisha Mimi,
Nimejeruhi, tena naponya. (K)

Nikiuonoa upanga wangu wa umeme,
Mkono wangu ukishika hukumu,
Nitawatoza kisasi adui zangu,
Nitawalipa wanaonichukia. (K)


SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu, na kulishika.
Aleluya.


INJILI
Mt. 16:24-28

Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 

Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake. 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo


Copyright © 2026 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment