Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA IJUMAA, AGOSTI 23, 2024



MASOMO YA MISA, IJUMAA, AGOSTI 23, 2024
JUMA LA 20 LA MWAKA


SOMO 1
Eze. 37:1 – 14

Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana.

Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana Mungu, wajua wewe. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana Mungu aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, teteme3ko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake, lakini haikuwamo pumzi ndani yake. Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana Mungu asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi. Basi nikatabiri kama alivyoiamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.

Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa. Basi tabiri, uwaambie Bwana Mungu asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza asema Bwana.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 107:1 – 9 (K) 1

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.

Waseme hivi waliokombolewa na Bwana,
Wale waliowakomboa na mkono wa mtesi.
Akawakusanya kutoka nchi zote,
Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. (K)

Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika;
Hawakuona mji wa kukaa.
Waliona njaa, waliona na kiu,
Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. (K)

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao,
Akawaponya na shida zao.
Akawaongoza kwa njia ya kunyoka,
Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.(K)

Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake,
Na maajabu yake kwa wanadamu.
Maana hushibisha nafsi yenye shauku,
Na nafsi yenye njaa huijaza mema. (K)


SHANGILIO
Zab. 111:7, 8

Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, ee Bwana, 
ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya.


INJILI
Mt. 22:34 – 40

Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment