Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA ALHAMISI, AGOSTI 20, 2026



MASOMO YA MISA 
ALHAMISI, AGOSTI 20, 2026
JUMA LA 20 LA MWAKA


SOMO 1
Eze. 36:23 – 28

Neno la Bwana linifikia hivi: Nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana Mungu, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nayi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.

Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia rohoyangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nayi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51:10: - 13, 16 – 17 (K) Eze. 36:25

(K) Nitawanyunyizia maji safi, Nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau. (K)



SHANGILIO
Zab. 19:8

Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.



INJILI
Mt. 22:1 – 14

Yesu aliwaambia makuhani na makutano kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa waake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu, ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusi. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.

Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakin wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.

Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment