Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 8, 2022



MASOMO YA MISA, JULAI 8, 2022
IJUMAA, JUMA LA 14 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Hos. 14: 2 – 9

Bwana anasema: Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyiroro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni.

Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.

Efraimu atasema, Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, name nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako.

Ni nani aliey na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliey na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51: 1 – 2, 6 – 7, 10 – 11, 15 (K) 15

(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)

Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni,
Nawe utanijulisha hekima kwa siri,
Unisafishe kwa hisopo name nitakuwa safi,
Unioshe, name nitakuwa mweupe kuliko theluji. (K)

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa change kitazinena sifa zako. (K)


SHANGILIO
1 Pet. 1:25

Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.


INJILI
Mt. 10: 16 – 23

Yesu aliwaambia mitume wake: Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.

Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu ndani yenu.

Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2022. These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.



No comments:

Post a Comment