MASOMO YA MISA, AGOSTI 1, 2024
ALHAMISI, JUMA LA 17 LA MWAKA
ALHAMISI, JUMA LA 17 LA MWAKA
SOMO 1
Yer. 18:1 – 6
Neno hili ndilo lilomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu. Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfainyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya.
Ndipo neno la Bwana likamjia, kusema, Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 146:1 – 5 (K) 5
(K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.
Ee nafsi yangu umsifu Bwana,
Nitamsifu Bwana muda ninaoishi,
Nitamwimbia Mungu wangu ningali hai. (K)
Msiwatumainie wakuu,
Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.
Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake,
Siku hiyo mawazo yake yapotea. (K)
Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake.
Aliyezifanya mbingu na nchi,
Bahari na vitu vyote vilivyomo. (K)
SHANGILIO
1 Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:47 – 53
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.
Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
No comments:
Post a Comment