MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2022
JUMANNE, JUMA LA 17 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA WAT. YOAKIM NA ANNA, WAZAZI WA BIKIRA MARIA
SOMO 1
Ybs. 44:1, 10 – 15
Haya na tuwasifu watu wa utauwa, Na baba zetu katika vizazi vyao. Lakini hawa walikuwa watu wa utauwa, wala kazi zao za haki hazisahauliki. Wema wao utawadumia wazao wao, Na urithi wao una wana wa wana;
Wazao wao wanashikamana na agano, Na watoto wao kwa ajili yao. Kumbukumbu lao litadumu milele, Wala haki yao haifutiki kamwe; Miili yao imezikwa katika amani, Na jina lao laishi hata vizazi vyote. Mkutano wa watu wataitangaza hekima yao, Na makusanyiko watazihubiri sifa zao.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 132:11, 13 – 14, 17 – 18
(K) Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
Bwana amemwapia Daudi neno la kweli,
Hatarudi nyuma akalihalifu,
Baadhi ya wazao wa mwili wako
Nitawaweka katika kiti chako cha enzi. (K)
Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni,
Ameitamani akae ndani yake.
Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)
Hapo nitamchipushia Daudi pembe,
Na taa nimemtengenezea masihi wangu.
Adui zake nitawavika aibu,
Bali juu yake taji yake itasitawi. (K)
SHANGILIO
Lk. 2:15
Aleluya, aleluya,
Waliitarajia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yao.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:16 – 17
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2022 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment