MASOMO YA MISA, JULAI 25, 2024
ALHAMISI, JUMA LA 16 LA MWAKA
SIKUKUU YA MT. YAKOBO, MTUME
SOMO 1
2 Kor. 4:7 – 15
Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu
ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali
hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi;
twatupwa chini, bali hatuangamizwi; sikuzote twachukua katika mwili kuuawa
kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana
sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu
nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya
kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu.
Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama
ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na
kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu
atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana
mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio
wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126 (K) 5
(K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha.
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha. (K)
Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
SHANGILIO
Yn. 15:16
Aleluya, aleluya,
Ni mimi niliyewachagua ninyi nikawaweka mwende mkazae
matunda, na matunda yenu yapate kukaa, asema Bwana.
Aleluya.
INJILI
Mt. 2:20 – 28
Mama yao wana wa Zebedayo alimwendea pamoja na wanawe,
akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza
kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono
wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba.
Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.
Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa
kuume na mkono wangu wa kushoto sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa
tayari na Baba yangu.
Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia ndugu wawili.
Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa
nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu
yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote
anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu
asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment