Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 22, 2023


MASOMO YA MISA, JULAI 22, 2023
SIKUKUU YA MT. MARIA MAGDALENA


SOMO 1
Wim. 3 :1-4

Usiku kitandani nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nalimtafuta, nisimpate. Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu.

Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu

Au

SOMO 1
2 Kor. 5 :14-17

Upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.

Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena, Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya.

Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu



WIMBO WA KATIKATI
Zab 63: 1-5, 7-8 (K) 1

(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji. (K)

Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu. (K)

Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. (K)

Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu inakuandama sana;
Mkono wako wa kuume unanitegemeza. (K)



SHANGILIO

Aleluya, aleluya, Maria tuambie: sema uliyoona njiani. Kaburi lilimfadhi yule aliye Mzima; Niliona utukufu wa Kristu alipokuwa akifufuka. Aleluya.



INJILI
Yn. 20 :1-2, 11-18

Siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka

Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment