MASOMO YA MISA, JULAI 21, 2022
ALHAMISI, JUMA LA 16 LA MWAKA
SOMO 1
Yer. 2:1-3, 7-8, 12-13
Neno la Bwana likanijia, kusema, Enenda ukalie masikioni
mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakumbuka hisani ya ujana wako,
upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuaata huko jangwani, katika nchi
isiyopandwa mbegu. Israeli walikuwa utakatifu kwa Bwana; Malimbuko ya uzao
wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajilia; asema Bwana.
Nami nitawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda
yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi
nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo. Makuhani hawakusema, Yuko
wapi Bwana? Wala wanasheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii
walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.
Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope
sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana. Kwa maana watu wangu hawa wametenda
maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia
mabirika, mabirika yavunjayo, yasiyoweza kuweka maji.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 36:5 – 10 (K) 9
(K) Kwako Bwana iko chemchemi ya uzima.
Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni,
Uaminifu wako hata mawinguni.
Haki yako ni kama milimo ya Mungu,
Hukumu zako ni vilindi vikuu. (K)
Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.
Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhila zako! Wanadamu
huukimbilia uvuli wa mbawa zako.
Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako,
Nawe utawanywesha mto wa furaha zako. (K)
Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima,
Katika nuru yako tutaona nuru.
Uwadumishie wakujuao fadhili zako,
Na wanyofu wa moyo uaminifu wako. (K)
SHANGILIO
Zab. 147:12, 15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya
nchi.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:10 – 17
Wanafunzi walimwambia Yesu, Kwa nini wasema nao kwa
mifano? Akajibu akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni,
bali wao hawakujaliwa. Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa
tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alichonacho hata kile alicho
nancho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano kwa kuwa wakitazama
hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia
kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala
hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, na kwa masikio yao hawasikii
vema, na macho yao wameyafumba; wasije wakaona
kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao,
wakaongoka, nikawaponya.
Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio
yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye
haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone na kuyasikia mnayoyasikia
ninyi, wasiyasikie.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2022 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment