MASOMO YA MISA, JUNI 30, 2022
ALHAMISI, JUMA LA 13 LA
MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Amo. 7:10 – 17
Amazia kuhani wa Betheli, alipeleka habari kwa Yeroboamu,
mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya
Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote. Kwa maana Amosi asema hivi,
Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya
kufungwa, atoke katika nchi yake. Tena Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwona,
nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini
usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni
nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii,
wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye
Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwabarie
watu wangu Israeli.
Basi, sasa lisikie neno la Bwana; Wewe unasema,
Usitabiri, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya
Isaka; kwa hiyo, Bwana asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana
wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa
kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli
atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19: 7 – 10 (K) 9
(K) Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
humtia mjinga hekima.
Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo. (K)
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
kinadumu milele. (K)
Hukumu za Bwana ni kweli,
zina haki kabisa. (K)
Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:105
Aleluya, aleluya.
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
INJILI
Yesu alipanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na
tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona
imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu;
umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao,
Huyu anakufuru. Naye Yesu hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu
mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au
ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo
amri duniani ya kusamehe dhambi, (akamwambia yule mwenye kupooza) Ondoka,
ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa
na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment