MASOMO YA MISA, JULAI 2, 2024
JUMANNE, JUMA LA 13 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Am. 3:1-8;11-12
Lisikieni neno hili alilolisema Bwana juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema, Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote.
Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Je! Simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwanasimba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu? Je! Ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu chochote? Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta Bwana? Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amekwisha kuunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana Mungu amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri? Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana. Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli; na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 5:4 – 7 (K)8
(K) Bwana uniongoze kwa haki yako.
Huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
Mtu mwovu hatakaa kwako;
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako. (K)
Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila. (K)
Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako,
Nitaingia nyumbani mwako;
Na kusujudu kwa kicho,
Nikilielekea hekalu lako takatifu. (K)
SHANGILIO
Yn. 15:15
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema, Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 8:23-27
Mt. 8:23-27
Yesu alipanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.©, These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment