MASOMO YA MISA, APRILI 28, 2017
IJUMAA, JUMA LA 2 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo 5:34-42
Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli,
mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza,
akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli,
jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi
aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne
wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si
kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha,
akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote
waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa,
waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu,
itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana
kuwa mnapigana na Mungu. Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume,
wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende
zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa
wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. Na kila siku, ndani ya hekalu na
nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni
Kristo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Bwana.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 27:1, 4, 13-14
(K)Neno moja nimelitaka kwa Bwana, Nikae
nyumbani mwa Bwana.
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)
Neno Moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SHANGILIO
Kol. 3:1
Aleluya, aleluya.
Mkiwa mmefufuliwa na Kristo, yatafuteni yaliyo
juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
INJILI
Yn 6:1-15
Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya
Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa
sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani,
akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa
karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake,
alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena
ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate
ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake
mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna
mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi
kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani
tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa
ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki
kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni
vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu
kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale
waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu
ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka
kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke
yake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment