“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Agosti 16, 2021
Juma la 20 la Mwaka
Amu 2: 11-19
Zab. 106: 34-37, 39-40,
43-44 (K) 4
Mt. 19: 16-22
___________________
Ukigusa tutakosana.
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
tunakutana na wana wa Israeli wakidumbukia katika mateso na matendo ambayo
Yoshua kabla ya kifo chake aliwahi kuwaonya kwamba wasiyatende ili basi wapate
usalama toka kwa Mwenyezi Mungu.
Ukweli ni kwamba Israeli
alisahau na kuonesha majivuno, alisahau kila alichowahi kutendewa, na kilichowafanya
wasahau kirahisi ni kwamba walikuwa katika nchi ya ahadi ambapo walikuwa na
kila kitu. Walikuwa na chakula, amani na vya kutosha. Hivyo walimsahau Mungu
kirahisi sana na kuanza kujishikiza na watu wa mataifa mengine.
Sisi tunaposikia maneno
haya, yafaa tutambue umuhimu wa kukumbuka historia ya maisha yetu, historia ya
taifa letu na pia ya wazazi wetu. Wana wa Israeli waliokuwa katika nchi ya
ahadi waligeukia miungu mingine kirahisi kwa sababu wengi kati yao walizaliwa
katika nchi ya ahadi na hawakubahatika kuyaona matendo makuu ya Mungu
aliyoyatenda wakati wazazi wao walipokuwa jangwani.
Hivyo pale walipoelezwa
historia ya taifa lao, na juu ya ukuu wa Mungu na ulazima wa kuyafuata mausia
ya Mungu, wao hawakuheshimu bali walipuuzia na hivyo wakapatwa na magumu
tuyasikiayo katika somo la kwanza leo. Mambo ya namna hii yanakipata na kizazi
chetu cha sasa ndugu zangu. wengi kati yetu tunapuuzia, tukielezwa kitu na
wazee wetu hatuamini, tunajidai kuwa watu wa sayansi, watu wenye kuamini kile
tulichoona au kushuhudia kwa macho. Mambo ya namna hii yanatufanya tushindwe
kufuata maongozi ya wazee wetu na kubarikiwa. Tujifunze kuwatii wakubwa wetu,
na tujifunze toka kwa historia za wazazi, taifa na za maisha yetu kwa ujumla.
Katika somo la injili,
huyu kijana anayemfuata Yesu anaonesha hali ya ajabu kabisa. Ni kwa sababu ni
mara ya kwanza katika injili ambapo anayekuja kwa Yesu ameshindwa kurudi akiwa
na furaha. Amerudi akiwa na huzuni. Hili ni la kushtusha kidogo. Wengi
wanaokutana na Yesu wanarudi wakiwa na amani na furaha. Kwa nini huyu alirudi
akiwa na huzuni? Ni kwa sababu mbele ya Yesu alikwenda bila kujiachia. Tayari
alikuwa ameshikilia maslahi yake, mambo ambayo alimweleza Yesu kwamba ikiwa
utayagusa haya tutakosana. Haya mengine gusa, lakini ukigusha haya, tutakosana.
Na moja kwa moja Yesu anayagusa na hakika anashindwa kijana anashinda kupokea.
Sisi nasi tuna mambo ya
namna hiyo. Yapo ambayo huwa tunasema haya yasiguswe. Ukigusa tutakosana. Mambo
ya namna hii hakika ndiyo yanayotuangusha. Tuwe tayari kujichunguza ni mambo ya
namna gani na hivyo tupate kuyaachilia. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment