“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Agosti 17, 2021
Juma la 20 la Mwaka
Amu 6: 11-24
Zab. 85: 8, 10-13
Mt. 19: 23-30
Ni yule anayejali mali
kuliko Mungu.
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo
katika somo la kwanza Mwenyezi Mungu anawakumbuka wana wa Israeli wakiwa katika
nchi yao ya ahadi. Huku katika nchi ya ahadi, hawafurahii kama walivyofikiria
pale mwanzo kwamba itakuwa sehemu ya kula na kunywa maziwa na asali. Wanajikuta
tena wakiwa tena watumwa ndani ya nchi yao wenyewe waliopewa na Bwana. Yote
haya ni kwa sababu ya kiburi chao ndugu zangu.
Wao wamemwacha Bwana
Mungu wa Israeli na kwenda kuitumikia miungu mingine. Ndipo walipojikuta
wakiingia katika utumwa. Ndugu zangu, wana wa Israeli walikombolewa sio tu
kimwili bali kiroho pia. Mwenyezi Mungu alipowatembelea kule Misri,
hakuwakomboa kimwili tu, bali aliwapatia pia ukombozi wa kiroho, Mwenyezi Mungu
alipata kujitambulisha kwao kuwa ndiye Mungu wao, na hivyo akawaokoa katika
utawala wa Ibilisi. Kosa la wana wa Israeli ni kwamba wao walikuwa
wakijirudisha katika utumwa kwa kuanza kuiabudu tena miungu ya kipagani na
sanamu. Utumwa huu uliwafanya pia watekwe kimwili. Hivyo walipaswa kujitoa
katika utumwa wa kiroho, wazipatie roho zao uhuru na ndipo pia waipatie miili yao
ukombozi pia.
Sisi ndugu zangu tutambue
kwamba tutakuwa na ukombozi kweli pale tutakapothamini ukombozi wetu wa
kiroho.Tutakapozikabidhi nafsi zetu kwa shetani tena ndipo tutakapokuwa watumwa
kwa kila kitu. Jamii yetu, familia itakuwa watumwa. Tutajisikia watumwa wa kila
kitu. Hivyo kila mmoja wetu tujitahidi kudumisha na kuupenda uhuru wetu wa
kiroho. Huu ndio ukombozi wa kweli.
Katika somo la injili,
Yesu anaelezea juu ya ugumu uliopo kwa tajiri kuingia katika ufalme wa
mbinguni. Anaeleza hili kwa kusema kwamba ni rahisi hata kwa ngamia kupenya
katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni,
tujiulize, tajiri ni mtu gani? Ni yule anayejali mali kuliko Mungu. Hivyo
ataona afadhali atumie muda wake kwa biashara zaidi kuliko kwa ajili ya Mungu.
Machoni pake faida ni kubwa kuliko utu wa mwanadamu mwenzake. Anaona thamani
katika mali yake kuliko katika mwanadamu mwenzake, yuko tayari kumwona mwenzake
anakufa njaa kuliko kumpatia kidogo ambacho kingalimpatia uhai. Huyu ndiye
tajiri; mwenye kuona thamani katika mali kuliko katika wanadamu wenzake au
katika Bwana.
Watu wa namna hii sio
lazima wawe na mali nyingi; wapo ombaomba wenye roho za namna hii. Hawa pia
itawawia vigumu kwao kuingia katika utawala wa mbinguni. Tunapaswa kuwa na roho
ya ukarimu, yenye kumjali Mwenyezi Mungu na jirani zetu pia. Hapa tutaweza
kuzikomboa roho zetu na utumwa wa mali.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment