“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumapili, Agosti 15 2021
Juma la 19 la Mwaka
SIKUKUU YA KUPALIZWA
BIKIRA MARIA MBINGUNI
Ufu 11:19, 12:1-6, 10;
Zab 45:9-11, 15 (K) 10;
1Kor 15:20-26;
Lk 1:39-56
MALENGO YA JITIHADA ZETU!
Karibuni ndugu zangu kwa
adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo ikiwa leo tunaadhimisha sherehe kubwa
katika kanisa; kupalizwa mbinguni kwake Bikira Maria. Hii ni siku ya ushindi
mkubwa kwake; Mama yake Mkombozi ametukuzwa. Alivumilia mengi pamoja na
Yesu:-tangu akubali kumchukua mimba licha ya kwamba alikuwa na mchumba tayari
(hapa alihatarisha maisha yake lakini hakuona shaka, alikuwa tayari kufa kwa
ajili ya Yesu), tangu kukimbilia na Yesu Misri, kumtunza na kumtafuta alipokuwa
amepotea, halafu Yosefu alikufa mapema na kumwacha mjana na ugumu wa kutunza
nyumba yake.
Halafu akaungana na Yesu
kwenye utume wake tangu alipokuwa anauanza hadi anakufa msalabani. Akashiriki
vyema kwenye kulianzisha kanisa la mwanzo na kuwa mshauri mkuu wa hii jumuiya
ya mwanzo ya Kikristo. Hii ndiyo shughuli aliyoifanya Bikira Maria.
Japokuwa kwenye Biblia
hakuna maelezo ya moja kwa moja juu ya kupalizwa mbinguni Bikira Maria, ukweli
ni kwamba lile kanisa la mwanzo lilishuhudia hili tukio na kutuandikia maelezo
muhimu kuhusu mwili wake kutokuoza kaburini. Wao walishuhudia kabisa na hivyo
basi walianzisha ibada mbalimbali za Bikira Maria wakimuona Mama Maria kama
mwombezi wa kanisa lao la mwanzo. Ukweli ni kwamba lile kanisa la mwanzo
lilipata msaada mkubwa sana kwa kumuomba Mama huyu na ibada kwa Mama huyu
haikuishia kwenye kanisa la mwanzo tu. Ilieendelea hadi kukaja kuwa na ibada
nyingine za Rozari na zote hizo zilizidi kutokea kadiri ya miaka ilivyokuwa
inasonga mbele.
Ndugu zangu, tukijaribu
kutafakari kuhusu Bikira Maria; jinsi ibada juu yake ilivyoanza na hadi hapa
tulipo, kweli bila ya kuwa na upendeleo wowote kweli hatuwezi kusema ati ibada
kwa Bikria Maria ni za kutunga tu. Kweli kama haya yote yangekuwa ni hadithi,
ungekuta yamekwishatoweka. Lakini cha ajabu ni kwamba kila kukicha, ibada hii
ndipo inapozidi kupata nguvu kila wakati. Kweli kwa Imani na msistizo jamani;
Mama huyu kweli astahili kuheshimiwa na kupewa nafasi katika kanisa.
Kingine ni kwamba
kupalizwa mbinguni Bikira Maria ni nafasi au upendeleo aliopewa yeye kama yeye.
Kama kweli aliweza kupendelewa na kuwa mama wa Mungu, basi anaweza kupendelewa
na kupalizwa mbinguni na ndivyo ilivyokuwa. Yesu ana uwezo wa kumpaliza na
kweli alimpaliza.
Kupalizwa kwake kulikuwa
ni kwa faida yetu. Hii ni kwa sababu huko mbinguni anakuwa ni mwombezi wetu na
sio kwamba ati huko anakwenda kutesa na kupiga watu. Amepewa nafasi ambayo basi
atakuwa mwombezi wa kanisa na taifa kwa ujumla.
Wapo baadhi wanaopinga
kupalizwa Mbinguni Bikira Maria. Wanasema haiwezekani. Lakini nawaambieni
kwamba Mungu anauwezo wa kumpaliza na ndivyo alivyoweza kufanya. Hivyo basi leo
tuongeze ibada kwa Mama yetu. Leo kapalizwa ili akawe mwombezi wetu. Tumwelekee
huko basi tuweze kupata msaada na maombezi yake. Amina.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment